BREAKING NEWS: Rais Magufuli akutana viongozi wa dini Ikulu


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt



Dar es Salaam. Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini za kikristo nchini.
Katika mazungumzo yao Rais amewataka kufanya kazi na kuendelea kuhubiri kuhusu amani, upendo na mshikamano.
“Nawahakikishia mimi nipo pamoja na nyinyi, nendeni mkafanye kazi kwa kujiamini na kwa uhuru, mkiwa na jambo lolote nijulisheni nitalishughulikia, wahubirieni Watanzania amani, upendo, mshikamano na kuipenda nchi yao,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Agosti, 7 2018 alipokutana na viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) waliokwenda Ikulu jijini Dar es Salaam kujitambulisha kwake.
Viongozi hao ni pamoja na Mwenyekiti wa CCT Askofu Anilikisa Cheyo, Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti  wa CCT Askofu Fredrick Shoo, Makamu wa Pili wa Mwenyekiti CCT Askofu Jacob Chimeledya na Katibu Mkuu wa CCT Mchungaji Moses Matonya.
Wengine ni Rais wa TEC Askofu Gervas Nyaisonga NA  Makamu wa Rais TEC Askofu Flavian Kasalla..
Taarifa kutoka KWA Mkurugenzi wa Mawasiliano IkulU, Gerson Msigwa imesema kuwa  Rais  amekutana na kujadilina na viongozi hao kuhusu ushirikiano.
Rais Magufuli amewashukuru kwa dhamira yao ya kutaka kukutana nae na kufanya naye mazungumzo na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa madhehebu ya dini na taasisi zake.
Amesema serikali itaendelea kushirikiana nayo katika kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi.
 Anaeleza katika mazungumzo hayo viongozi hao wamemhakikishia utayari wao wa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali, kuyasimamia makanisa yao ili yaendelee kutoa huduma ya kiroho na kijamii kwa manufaa ya Watanzania wote na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Pia viongozi hao wamempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya wamu ya tano katika kuleta maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafiri na majengo, kuleta nidhamu katika utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa.
“Wamempongeza pia kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za Taifa hasa madini, kupambana na wizi na ufisadi wa mali za umma, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kuimarisha huduma za afya na  kuwapigania wakulima,” imesema taarifa hiyo
Viongozi hao wamewaomba watanzania wote kumpa ushirikiano wa kila aina Rais Magufuli kwa kuwa wanatambua na wameona kazi nzuri  anayoifanya.
By Beatrice Moses, Mwananchi Dar es Salaam bkabojoka@mwananchi.co.tz



Comments

Popular Posts