HABARI: Mtibwa Sugar yajisalimisha kwa Santos.










Dar Es Salaam. UONGOZI wa  Mtibwa Sugar upo katika mazungumzo na klabu ya Santos ya Afrika Kusini ili kujua ni kiasi gani wanadaiwa ili walipe na kuendelea na maandalizi yao ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mtibwa Sugar  ilipigwa faini ya dola 1500 baada ya kushindwa kucheza mechi ya marudiano na Santos mwaka 2002 hivyo ili washiriki michuano ya sasa hivi walipotwaa ubingwa wa Kombe la FA waliamuriwa kulipa faini na kuwalipa Santos pesa ya maandalizi ya mechi hiyo ambayo bado haijafahamika.
Shirikisho la soka Tanzania (TFF) lilitangaza kuwasiliana na CAF kuhusu hatua za utatuzi wa changamoto hiyo na kupewa nyongeza ya wiki mbili ili kuhakikisha gharama zote zinalipwa kwa wakati.
Akizungumzia mchakato huo Katibu mipango wa Mtibwa Sugar, Abubakar Swabur alisema klabu yao inafanya mawasiliano na Santos ili kujua namna ya kufanya malipo na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ijayo.
"Taarifa hiyo ipo, tumeshirikiana na TFF ambao wametueleza yao nasi tumewaeleza yetu lakini kimsingi kwasasa tuko katika mzungumzo na Santos kuhusu gharama zao ili tukamilishe malipo kwani CAF tuliwalipa," alisema Swabur
"Uwezekano wa sisi kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo kwa namna tulivyojipanga naamini upo wazi na tutafanya hivyo pale tutakapokamilisha mazungumzo yetu na Santos ambayo naamini watakuwa na nafasi ya kutusikiliza na kukubaliana," alisema.


Comments