NEWS: Maandamano yaibuka Zimbabwe, mmoja auawa
Harare, Zimbabwe. Maandamano makubwa yameibuka kupinga matokeo ya uchaguzi wa kihistoria yanayoelekea kumpa ushindi Rais Emmerson Mnangagwa mara yalipotangazwa Jumatano Agosti Mosi, 2018 na mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa.
Mtu huyo amefariki baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji katika juhudi za kuzuia maandamano hayo ya wapinzani mjini Harare.
Uchaguzi huo, ambao ni wa kwanza tangu kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe alipoondolewa na jeshi mwaka jana, ulitarajiwa kuwapa Wazimbabwe fursa ya kufunika ukurasa wa utawala wa mkono wa chuma.
Lakini utulivu ulitoweka na watu kujawa hasira na vurugu pale mashabiki wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) kutangaza kwamba wameibiwa matokeo.
"Ulisema wewe ni bora kuliko Mugabe – wewe ni taswira ya Mugabe," alipiga kelele mmoja wa vijana walioandamana akiwa amevalia fulana nyeupe. "Tunataka usalama wa watu."
Matokeo rasmi yaliyotangazwa hadi kufikia Jumatano asubuhi yameonyesha kwamba chama tawala cha Zanu PF kimejizolea viti 110 kati ya majimbo 153 hivyo kuonyesha matarajio ya Mnangagwa kuibuka na ushindi wa kiti cha urais.
Wafuasi wa MDC walichoma matairi na kuharibu alama mbalimbali za barabarani wakati maandamano hayo yalipoenea kuanzia kwenye makao makuu ya chama hadi Harare.
Comments
Post a Comment