NEWS: Heche amjibu Waitara uenyekiti wa Mbowe
Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche
Dar es Salaam. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amesema hata wapinzani wote wakikimbilia CCM, mapambano ya wananchi kupigania haki zao hayataisha.
Pia amehoji kama aliyekuwa mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara aliyehamia CCM ameondoka kwa sababu ya uenyekiti wa Freeman Mbowe, ataweza kumtoa Rais John Magufuli kwenye uenyekiti wa CCM?
“Ngoja nimuulize Waitara, kama ameondoka Chadema kwa sababu ya mwenyekiti na ameshindwa kumtoa Mbowe, ataweza kumtoa Magufuli?” amehoji mbunge huyo.
Heche aliyasema hayo jana akizungumzia kujiuzulu na kuhamia CCM kwa Waitara.
Julai 28, Waitara alitangaza kujivua ubunge na kuhamia CCM akitaja sababu mbalimbali ikiwamo uenyekiti wa Mbowe.
Pamoja na Waitara, mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga naye alitangaza kujiuzulu uanachama na wadhifa wake.
Akizungumza katika mkutano maalumu wa Jimbo la Ukonga, Heche alisema nia ya Chadema siyo kuwapa watu ubunge isipokuwa kuhakikisha inawasimamia wananchi katika kupata huduma bora ikiwamo elimu, afya, miundombinu na uchumi imara.
Alisema wananchi wa Ukonga walikesha siku tatu kupigania ushindi wa jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, lakini matokeo yake, Waitara amekimbia mapambano. “Hata kama CCM itanunua wapinzani wote, bado Watanzania wataendelea na mapambano, yeye ameenda kwa sababu ya masilahi yake lakini huku nyuma ameacha jeshi kubwa na tutampata mpambanaji mwengine atachukua jimbo,” alisema Heche.
“Niwaambie tu CCM hata mkininunua Heche leo, wananchi wataendelea kudai maendeleo yao, mtakuwa mmeninunua mimi hamjainunua Chadema.”
Kuhusu hoja ya Waitara kuwa Mbowe amekaa madarakani kwa muda mrefu, mbunge huyo alisema ni matakwa ya wanachama na sio ya CCM.
Alieleza kuwa katiba ya Chadema haijaweka ukomo wa uongozi na ataendelea kushikilia nafasi hiyo mpaka wanachama watakapotaka kumuondoa. “Kwani Mwalimu Nyerere (Julius) aliongoza kwa muda gani? Kwani Mbowe aliyeanza kuongoza mwaka 2006 amefikisha muda wa Mwalimu? Si bado? Basi nyie wanachama ndio wenye mamlaka na ndio mtakaomuweka mwenyekiti wa masilahi ya chama,” alisisitiza.
Heche alisema ni ajabu kuona kuwa Waitara anaondoka akidai moja ya sababu ni Mbowe kuongoza chama muda mrefu.
Alidai kuwa Waitara ni mwanasiasa wa siasa za mpasuko.
“Nimesikia anataka kuja Tarime kupambana na mimi mwaka 2020, namsubiri kwa hamu, siwezi kupambana na mamluki na haniwezi,” alisema.
“Ninawaambia wale wanaotaka kuondoka, milango ipo wazi, Chadema itaendelea kuwa imara.”
Diwani alia kupakaziwa
Awali, diwani wa Pugu, Boniventure Mphuru alidai kusikitishwa na taarifa zinazoenezwa kwamba naye ni miongoni mwa viongozi wa Chadema wanaotaka kuhamia CCM.
“Wananchi wa Ukonga puuzieni taarifa hizo, hazina ukweli kwa sababu sijawahi kuwa CCM, sitaenda na sijafikiria kwenda huko,” alisema.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Ukonga, Omary Swea alisema vitisho vya wabunge na madiwani kuhama chama hicho haviwatishi kwa sababu bado wako imara.
Alisema mkutano wa wanachama wa jimbo hilo walioufanya ni wa kawaida na upo kwenye katiba ya chama chao.
Naye mwenyekiti wa Mkoa wa Ilala wa chama hicho, Makongoro Mahanga alisema pamoja na vita waliyo nayo hawatakata tamaa wala kurudi nyuma.
Mdee ahojiwa polisi
Wakati huohuo, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, baadhi ya wanachama na wafanyabiashara wa eneo hilo walikamatwa na kuhojiwa na polisi jana, kwa kosa la kufanya mkusanyiko usio halali.
Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), alisema alipigiwa simu na vijana wanaofanya biashara ya kutengeneza bustani eneo la Mzimuni lililopo Kawe kwamba wamepewa notisi ya kuondoka.
Alisema wakati anapigiwa simu alikuwa Kunduchi katika ziara, hivyo ikamlazimu kwenda kuwasikiliza wananchi wake.
“Nilipofika nilizungumza nao na kuwaeleza suala hili nalishughulikia, kwani nimewasiliana na Wizara ya Ardhi; (Idara ya) Mipango Miji na Tarura (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini),” alisema.
“Ni kweli wale vijana wako eneo la barabara na wamenieleza hawana tatizo la kuondoka, lakini wanahitaji kuelekezwa wapi watakwenda kuendelea na shughuli zao.”
Mdee alisema baada ya kumaliza kuzungumza na vijana hao, aliondoka lakini alipofika mbele akaelezwa kuna watu wamekamatwa eneo alilotoka.
“Nikaona nirudi, nilipofika nikakuta wanarushwa kichura chura, nikahoji kuna nini sikupata majibu yanayoeleweka.”
Mdee alisema baada ya hapo, ikaelezwa kuwa vijana hao waliokuwa chini ya ulinzi watapelekwa kituo cha polisi Kawe na yeye akasema anatangulia kituoni.
“Nilipokuwa nakwenda kama mita 20 nikaambiwa na wewe mheshimiwa rudi, niliporudi nikaambiwa niko chini ya ulinzi na kuniweka katika gari yao, tukaenda hadi kituoni na kuhojiwa kwa kufanya mkusanyiko usiokuwa na kibali,” alisema mbunge huyo.
“Baada ya kuhojiwa, mimi na wale vijana lakini na wanachama wa Chadema wote tumeachiwa na tutajulishwa tena kama tutahitajika.”
Alipoulizwa juu ya kukamatwa kwa watu hao, kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumanne Murilo alikanusha akisema kazi ya Jeshi la Polisi ni kutoa huduma za kiusalama kwa mtu yeyote, hivyo si ajabu kwa kiongozi wa chama kufika katika kituo cha polisi inapobidi.
“Mtu yeyote akifika kituoni ina maana amekamatwa? Huyo Makene au Mbowe au Mdee akifika kituoni maana yake amekamatwa? Hilo ndilo swali langu,” alihoji.
“Hivyo watu wasitumie Jeshi la Polisi kujipatia umaarufu.”
Nyongeza na Cledo Michael.
Comments
Post a Comment