SPORT NEWS: Man United, Chelsea dili lao moja aisee!


LONDON, ENGLAND. Hili dili lipo na linavutia kweli kweli. Manchester United ina mpango wa kuipa ofa Chelsea wabadilishane mastaa wao, Anthony Martial aende Stamford Bridge na Willian atue Old Trafford. Kuna uwekano dili hilo likafanyika kabla ya Ijumaa.
Wote wawili hawana uhusiano mzuri na klabu zao kwa sasa huku wakiwa wanatamani kuhama. Martial amekuwa hana uhusiano mzuri na kocha wake, Jose Mourinho baada ya kutokomea kusikojulikana mara baada ya kwenda Ufaransa kushuhudia kuzaliwa kwa mtoto wake wa pili wa kiume.
Staa huyo alipigwa faini ya pauni 180,000 na United baada ya kushindwa kurudi tena nchini Marekani kuungana na wenzake mara baada ya kupata ruhusa ya kwenda Paris kushuhudia mpenzi wake akijifungua mtoto wa kiume.
Inasemakana aliwaambia wenzake kwamba hana mpango wa kurudi tena Marekani kitu ambacho kilimkasirisha Mourinho ambaye anataka kuachana na staa huyo huku akipata faida ya kumpata Willian kutoka Chelsea bila ya pesa yoyote kutumika.
Kwa muda mrefu Mourinho amekuwa akimsaka Willian ambaye alikuwa mchezaji staa zaidi katika msimu aliotimuliwa Chelsea baada ya timu hiyo kufanya vibaya na Willian yuko tayari kufanya kazi tena na kocha huyo Mreno.
Tayari WIllian naye amekuwa na majanga yake katika kikosi cha Chelsea chini ya kocha mpya, Maurizio Sarri ambaye alikerwa na kitendo cha nyota huyo kuchelewa kujiunga na kambi yake kwa madai ya tatizo la hati yake ya kusafiria.
Kocha Sarri ambaye amejiunga klabuni hapo akitokea Lazio ya Italia amekiri kutofurahishwa na kitendo cha nyota huyo wa kimataifa wa Brazil huku akidai kwamba anataka kufanya maongezi naye kuhusu tukio hilo na mustakabali wake kwa ujumla.
“Nataka kuongea naye. Sina furaha na hali ilivyo lakini kabla sijajibu chochote nataka kuongea naye.” Alisema kocha huyo ambaye jana kikosi chake kilitazamiwa kucheza mechi ya ufunguzi wa msimu na Manchester City.
Wachezaji wote wanathaminishwa dau la pauni 75 milioni lakini Martial anaonekana kuwa na thamani zaidi kwa vile ni mdogo kwa Willian kwa miaka saba na kuna uwezekano United wakadai chochote kutokana na tofauti hiyo.
Katika dirisha hili Willian alikaribia kujiunga na Barcelona lakini klabu hiyo ya Catalunya ikachemsha kutokana na dau kubwa ambalo Chelsea walikuwa wanalitaka. Badala yake waliamua kumchukua winga mahiri wa Kibrazil, Malcom kutoka Bordeaux ya Ufaransa.
Upande wa Martial, yeye kupitia kwa wakala wake alishatangaza kutaka kuondoka Manchester United katika siku za mwanzo za ufunguzi wa dirisha hili lakini United walipania kumbakisha kuhofia kufanya kosa kama ambalo Mourinho alilifanya wakati akiwaruhusu Kevin de Bruyne na Mohamed Salah waondoke Chelsea.
Juventus na Bayern Munich pia zimekuwa zikimsaka staa huyo ambaye kutokana na kucheza dakika chache msimu uliopita alishindwa kupata nafasi ya kuwemo katika kikosi cha kocha Didier Deschamps cha Ufaransa ambacho kilitwaa taji la kombe la dunia nchini Russia mwezi uliopita.
Endapo dili hilo litatokea, haitakuwa mara ya kwanza kwa United kufanya dili la kubadilishana wachezaji baada ya kufanya hivyo katika dirisha la Januari ambalo walimchukua staa wa kimataifa wa chile, Alexis Sanchez kutoka Arsenal huku wakiwapatia wababe hao wa London kiungo wa kimataifa wa Armenia, Henrikh Mkhitaryan.

Comments

Popular Posts