SPORT NEWS: Makambo kumalizana na Okwi tu uwanjani







STRAIKA mpya wa Yanga, Heritier Makambo ameanza uchokozi mapema akimtangazia vita Emmanuel Okwi aliyeibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita kwa mabao yake 20 na kuipa timu yake taji.
Okwi pamoja na John Bocco na Winga Shiza Kichuya katika utatu wao walifunga jumla ya mabao 41 na kuipa Simba ubingwa ikiuhamisha toka Jangwani, lakini Mkongo huyo aliyetua hivi karibuni akitokea FC Lupopo amechimba mkwara mzito.
Makambo alisema ametua Yanga kwa kazi moja tu ya kufunga, hivyo kama kuna washambuliaji waliotisha msimu uliopita kwa kutupia kambani waanze kuhesabu maumivu kwani amepania kuwafunika na kuisaidia timu yake kurejesha taji la Ligi.
Mshambuliaji huyo alisema kiu yake licha ya kuibeba Yanga, lakini pia anatamani awe Mfungaji Bora.
Makambo aliyepo kambini mjini Morogoro na kikosi cha Yanga kinchojifua kwenye Uwanja wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), alisema kama mambo yataenda vizuri anatamani afunge mabao mengi zaidi ya straika yeyote ili abebe kiatu.
"Kila mshambuliaji anatamani kuwa mfungaji bora, lakini kuna mmoja tu ambaye anawazidi wote, hata mimi nimepania kujituma ili kufunga mabao mengi na kunyakua kiatu cha Dhahabu, naamini naweza kwa uwezo wa Mungu," alisema.
Alipoulizwa idadi gani ya mabao anayojiwekea malengo, alijibu kwa kusema;
"Nadhani ni mapema kulizungumza hilo, ila nitafute mwisho wa msimu ili ujue nimefanikiwa kuchukua tuzo hiyo au la, ila nawaomba mashabiki wa timu yangu kuwa na imani na timu kwani bado tunaendelea kujenga kikosi na cha ushindani."
Makambo alinyakuliwa na Yanga kuchukua nafasi ya Obrey Chirwa aliyeondoka Jangwani, huku wakiiacha timu ikiwa haina mshambuliaji tegemeo wa kuifungia mabao katika michuano ya CAF. Hata hivyo ITC ilimkwamisha kuanza kuichezea.
By THOBIAS SEBASTIAN

Comments

Popular Posts